Na Olle Bergdahl Mjengwa,
MSOMAJI, sherehe za soka imeanza katika fukwe za Copacabana pale nchini Brazili.
Tanzania hawapo katika mashindano hayo na kwa hiyo wengi wetu tunashabikia timu tofauti tofauti katika fainali hizi za Kombe la Dunia. Wengi tunashabikia timu ambazo zina nafasi kubwa kushinda mashindano hayo. Ni timu kama vile England, Brazil na Argentina.
Lakini, naamini wengi wetu pia tunashabikia timu zetu za Afrika. Ni kwa kuwa wanatuwakilisha katika mishindano hayo.
Inafahamika, kwamba katika historia ya Kombe la Dunia hakuna timu ya Afrika ambayo imefikia nusu fainali ya mashindano hayo. Mwaka 2002 Senegal walifikia hatua ya tatu , na katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini, Ghana pia walifikia hatua ya tatu na walishindwa kufuzu kucheza nusu fainali kutokana na kutolewa kwa penalti na Uruguay.
Nina matumaini kwamba timu yetu moja ya Afrika itafika mbali katika fainali hizi za Kombe la dunia. Wiki iliyopita timu ya taifa ya Kameruni ama maarufu kama ' Simba wasiofugika' walifungwa na Mexico kwa bao moja kwa bila.
Kameruni sasa wana nafasi ndogo sana ya kufuzu hatua ya pili kutoka kundi A ambalo pia lina timu mwenyeji wa mashindano ya kombe la dunia, Brazil. Bila kusahau kuwa Kroatia pia wamo kwenye kundi hili.
Ingawa ' Simba wasiofugika' walishindwa kushinda mechi yao ya kwanza, 'Tembo' wa Ivory Coast walifanikiwa kushinda mechi yao dhidi ya Japan.
Msomaji, naongea kuhusu Ivory Coast. Nchi hii Ivovy Coast ina kizazi cha dhahabu. Wana wachezaji kama akina Drogba, Toure, Gervinho na Kalou. Lakini, kizazi hiki hakijashinda taji hata moja! Na hawajapata mafanikio katika fainali za Kombe la Dunia.
Fainali hizi za Kombe la Dunia ni nafasi ya mwisho kwa wachezaji wengi katika kizazi hiki cha dhahabu cha Ivory Coast kufanya makubwa. Yaya Toure ana miaka 31, Zakora ana miaka 34, na Didier Drogba ana miaka 36! Kama kuna mchezaji ambaye anastahili kupata mafanikio katika kombe la dunia, basi ni Didier Drogba.
Drogba ni mchezaji anayependwa zaidi nchini Ivory coast. Ni kutokana na mafanikio yake makubwa kimpira , lakini, pia kwa kuwa mchezaji huyu alisaidia kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe ndaniya Ivory Coast mwaka 2005. Ilikuwa ni baada ya mechi ya mwisho ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Ivory Coast walishinda mechi yao dhidi ya Gambia na katika vyumba vya kubadilishia nguo, Drogba akiwa mbele ya televesheni ya taifa alipiga magoti yake na aliomba pande zote zinazopigana vita kuacha kupigana na alieleza kwamba wachezaji wote wa Ivory Coast wanataka amani.
Wiki moja baada ya hapo Rais wa Ivory Coast na kiongozi wa waasi waliokuwa wanadhibiti eneo la kazkazini la Ivory Coast waliangalia kwa pamoja mechi ya Ivory Coast dhidi ya Madagaska katika mji wa Bouake!
Wiki moja tu kabla ya mechi hiyo wanajeshi wa viongozi hawa walikuwa wanapiga vita! Lakini, baada ya hotuba ya Drogba, wananchi wote, na pande zote zinazopigana walikubali kwamba wanahitaji amani.
Hivyo, Drogba alifanikiwa kuleta amani nchini Ivory Coast. Je, ataweza kuwapa Ivory Coast na Afrika mafanikio makubwa katika fainali za Kombe la Dunia?
Mwaka 1994 Colombia iliingia kwenye fainali za kombe la dunia kama moja ya nchi zilizotajwa kuwa zingeweza kunyakua kombe. Na hata Pele aliwatabiria hivyo. Lakini, Colombia waliyaaga mashindano kwenye hatua ya makundi tu. Ni baada ya kufungwa na Romania na Marekani.
Kufungwa na Marekani 2-1 kulifanya goli la kujifunga mwenyewe la beki Andreas Escobar ligharimu maisha yake. Siku kumi baada ya mechi ile, Escobar alimiminiwa risasi 12 wakati akiegesha gari yake nyumbani Colombia. Inasemwa muuaji alitumwa na wacheza kamari waliopoteza fedha nyingi kwa Escobar kusababisha goli. Maana, muuaji katika kila risasi aliyofytua, alisikika akitoa sauti kubwa ikisema "Goooli!"
Naam, Colombia soka inaweza kuwa suala la kufa na kupona..
Maggid,
No comments:
Post a Comment