Tuesday, 16 September 2014

BUNGE MAALUM LA KATIBA YAHITIMISHWA RASMI




Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dodoma
HOJA ya kusitisha Bunge Maalum la Katiba imehitimishwa rasmi Kisheria kwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutamka kwamba bunge hilo linaweza kuendelea na shughuli zake.
Taarifa hiyo imetolewa jana 15 Septemba, 2014 na Mjumbe wa Kamati namba Tano, Mhe. Dkt. Asha-Rose-Migiro wakati wa mjadala wa jioni bungeni hapo.
Akisoma taarifa hiyo, Dkt. Migiro amesema kuwa mjadala wa kusitisha bunge umefungwa rasmi hapo jana licha ya kuwepo kwa madai kuwa bunge hilo halina uhalali wa kisiasa.
"Kwaajili ya kuondoa shaka yoyote ningependa kuwaambieni takwimu tulizonazo hivi sasa, bunge hili lina jumla ya Wajumbe 630, kati ya hao waliotoka ni wajumbe 130 ambao ni sawa na asilimia 21% tu ya wajumbe wote, wajumbe waliobaki ndani ya bunge ni 500 hii ni sawa na asilimia 79% ya wajumbe wote na tukizichambua takwimu hizi, ningeomba kutambua wingi wa Kundi la 201", alisema Dkt. Migiro.
Akikanusha juu ya kuwepo kwa dhana iliyojitokeza ya kwamba wajumbe waliobaki ndani ya bunge hilo ni wa aina moja, Dkt. Migiro alisema kuwa taarifa hizo si za kweli, kwani kati ya wajumbe 500 walioko ndani ya bunge hilo wajumbe wanaotokana na kundi la 201 ni wajumbe 189 ambapo wajumbe wanaotoka Tanzania bara jumla yao ni 348 na kati ya hao, 125 ni wajumbe wanaotoka katika kundi hilo la 201.
"Ukitazama takwimu hizi kwa jicho lolote lile basi wajumbe wa 201 ni sehemu kubwa na ni sehemu muhimu ya wajumbe hawa waliobaki", alisema Dkt. Migiro.(Martha Magessa)

No comments:

Post a Comment