Tuesday, 24 June 2014

WALIOHUKUMIWA KUNYONGWA MPAKA KUFA, KWA KESI YA KUUA YA ALBINO



Marehemu  John Mwankenja, enzi za uhai wake
Kushoto ni mfungwa, Hakimu Mwakalinga ambaye ni mshtakiwa wa kwanza kuhukumiwa kunyongwa.
BAADHI ya wafungwa waliohukumiwa kunyongwa mpaka kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rungwe ambaye alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha waliohusika na mauaji ya albino wanaadhibiwa, wamefikishwa mahakamani leo katika mahakama ya wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

SAUTI KUTOKA NYIKANI.....SERIKALI INAJAZA MAJI YA BOMBA KWENYE KAPU LENYE MATUNDU

 GORDON KALULUNGA
BUNGE la bajeti linaendelea mjini Dodoma. Kabla ya kuhitimishwa watu wa nyikani wameniambia niwaeleze wabunge kuhusu tamaa niliyonayo ya kuwa mwalimu wao.
ieleweke kuwa, kila penye ufa au malalamiko ya watu, kuna watu wananufaika.
Waziri wa Fedha Saada Mkuya, amesema uchumi umekua kwa asilimia saba. Hapaswi kubishiwa Waziri huyu na serikali yake.
Asilimia saba ni uwiano tu, lakini ni zaidi ya hapo. Kila ambaye yupo kwenye kitengo, uchumi kwake umekua mara dufu na unaendelea kukua.
Kwanza ijulikane kuwa suala zima la ukusanyaji wa kodi ni gumu sana na lina gharama kubwa. Kasoro kodi za watumishi zinazokatwa kwenye mishahara.
Kuna makapu ya (plastic), yenye vitobo vingi, yanayotumika kuwekea takataka maofisini na nguo chafu kwa wenye uwezo wao.
Pamoja na Serikali kujipanga na kuendelea kukusanya kodi licha ya kuwepo misamaha mingi kwa wafanyabiashara wakubwa huku akina mama wauza mboga za majani wakitozwa kodi kila siku, tatizo lililopo ni ukusanyaji ambao ni sawa na kufungulia bomba, matarajio yakiwa ni kujaza maji kwenye kapu lenye matobo mengi.
Watu wengi kwa sasa wanataka kufanyia TRA au kwenye idara za manunuzi (Procurement) kwa madai kuwa huko wanatoka haraka.
Hayo ni moja ya makapu ya serikali yaliyo na matundu mengi kwa waliopewa dhamana, huku serikali ikikazana kufungulia maji bombani huku ikiwa imekinga makapu hayo.
Ngoja niachane na jambo hili, maana wahusika wanajua fika kuwa najisumbua, kwasababu hakuna wa kuwawajibisha kwa vitendo katika nyika yetu.
Kabla ya kumalizika kikao cha Bunge la bajeti, natamani kuwa Mwalimu katika shule iitwayo Bunge na wanafunzi waitwao waBungwe. Kabla ya kumaliza vikao ningempa kila mmoja kazi yake ya kufanya nyumbani (jimboni).
Baadhi nina uhakika kuwa wangefaulu vizuri ingawa sisemi kuwa wengine wangefeli. Singida mjini Mohamed Dewji, Zungu,  Monduli Edward Lowassa na wewe, sijui kwanini nimewataja viongozi hawa kwa majina, lakini tuliache kama lilivyojitokeza.
Ingenichukua muda kusahihisha kazi hizo za nyumbani (Homeworks), lakini wote wangefanya vema, Tanzania yangu ingekuwa sehemu bora ya kuishi kuliko ilivyo sasa.
Napenda mfumo wa ufundishaji wa walimu wa zamani "old style" ya ualimu. Ile waliyokuwa wakiifanya waalimu kama Baba yangu Mwalimu mstaafu, Frank Burton Kalulunga, ambapo walimu walikuwa wanajua uwezo wa kila mwanafunzi.
Walikuwa wanahakikisha kuwa kila mwanafunzi anafanya kazi aliyopewa na walikuwa wanasahihisha siku inayofuata.
Walikuwa na uwezo wa kutambua kama mwanafunzi kafanya mwenyewe ama amefanyiwa. Baada ya kusahisha, walikuwa wakibandika matokeo.
Shabaha ilikuwa ni kujua nani kawa wa kwanza na nani wa mwisho. Hapo ilikuwa ni lazima mwanafunzi asome sana ili aweze kupata Vema.
Mfumo ule ulikuwa na faida, maana yaliyotendeka ilikuwa ni changamoto kwa kila mwanafunzi kuongeza juhudi katika masomo.
Mfumo huu ningeupata na kuweza kuutumia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naamini ingesaidia sana.
Ningehakikisha kila Mbunge anapoondoka bungeni baada ya kusanyiko anapewa kazi ya kufanya jimboni mwake na akirejea "darasani" (kikao) kijacho, kwanza ninaangalia nani kafanya nini na kafanikiwa mangapi kisha tunasonga mbele.
Lengo ni kujua nani anajua na kutatua matatizo ya jimboni mwake na kuwasaidia wapiga kura wake na pia tungejua nani hana ajualo kuhusu shida na mahitaji halisi ya waliomchagua.
Ingetuwezesha kujua nani yuko mstari wa mbele kubadilishana mawazo pale nitakapowapa kazi za makundi, kukokotoa maswali na kutumia maarifa ya wenzake kufanya kazi zake kuwasaidia wapiga kura wake.
Nina uhakika kwa mfumo huu lazima nchi yangu ingeinuka na kuanza kusimama dede na kutupa mguu mbele kuelekea kwenye mafanikio ya mahitaji halisi ya wapiga kura.
Licha ya kuwapa hizo kazi za nyumbani, ningewapa wabunge (wanafunzi) wangu, jukumu la kusaka mahitaji ya wahitaji ambao kwa bahati mbaya baadhi wameonekana kujisahau kuyaweka bayana.
Nigejaribu kuwashawishi "maafisa elimu" kuhakikisha mchujo wa kujiunga na shule (uchaguzi) unafanyika kwa nyakati tofauti kwa faida na sababu nilizozieleza.
Ningewapa mtihani wa kila Mbunge kuwa na kiwango cha chini cha kuishi jimboni mwake kila mwaka, kwasababu wapo wabunge ambao wanaenda majimboni kwa nadra sana.
Mtihani mwingine ungekuwa ni kushinikiza wabunge kufanya mikutano sehemu zote ambazo waliomba kura kabla na baada ya kuhudhuria vikao vya bunge.
Wengi wanapokutana bungeni wanasema mahitaji ya jimbo sijajua kwa mujibu wa nani,(sisemi kwa mujibu wa wananchi na wala sisemi kwa mujibu wa wao).
Sina imani kwa sasa kama wabunge wanapoondoka bungeni kama wanapewa majukumu ya kutekeleza, ama wakipewa wanaweza kuyatekeleza bila kuwaeleza wananchi? Lakini kama ni majukumu kwa wananchi si tungeona mabadiliko huko tuliko?
Namaanisha hata kama hatuambiwi si tungejua kuwa "ujenzi wa hizi zahanati ni manufaa ya m'bunge kwenda kwenye kikao / vikao vya mwaka huu?
Kuna mwananchi anayeweza kujibu akiulizwa amenufaika nini na m'bunge wake kwenda kwenye vikao vya kila mwaka? Sisemi hatujanufaika, (japokuwa sisemi kuwa tumenufaika), sijui tufikirieje matumizi ya kodi zetu?
Kama mwalimu, ningehakikisha maswali yanajibiwa na kazi zangu zote zingefanyika na naamini mwisho wa muhula ningebandika matokeo, pia kuyatuma kwa wazazi (wananchi) ili wajue maendeleo ya wanafunzi na kujua nini cha kuwafanya katika muhula ujao wa shule (mhula wa uchaguzi).

No comments:

Post a Comment