Friday, 20 June 2014

Nge alinifanya nijihamishe kambi ya JKT...!

2_5d511.jpg

Ndugu zangu,
Leo nilikutana na ndugu yangu mmoja tuliyekuwa naye JKT enzi hizo za Operesheni Kambarage- 90-91. Basi, tukakumbushana maisha yale ya JKT.
Naye ikawa mara ya kwanza kujua, kuwa ni kwanini, baadhi yetu, tulipokatwa bogi kutoka Itende JKT, Mbeya na kwenda detach ya Itaka, Mbozi, kuwa mimi sikukaa kwenye kambi hiyo ya Itaka zaidi ya saa 48.
Itaka kulikuwa na mazingira magumu sana. Hanga hazikuwa na madirisha wala milango. Hakukuwa na umeme, hivyo hakukuwa na taa usiku. Tulichokifanya ni kutandika vitanda asubuhi, usiku ulipoingia ilikuwa ni kukitafuta kitanda chako kwa kuhesabu kwa kushika kwa mkono kuanzia cha kwanza hadi kitandani kwako.
Usiku mmoja tukamsikia mwenzetu akitoa sauti ya maumivu makali kuashiria kuna kilichomuuuma. Fumba na kuvumbua, askari wote tulishatoka nje. Kuna waliotokea mlangoni, na kuna waliotokea dirishani. Tuliamini kuwa tumeingiliwa na nyoka.
Tochi ilipopatikana ndipo akaonekana nge mkubwa na wa kutisha, Usiku huo sikulala kwa amani. Ilikuwa msimu wa masika na barabara ni mbaya sana. Lakini, kulipokucha nilisamehe chai na jioni ya siku hiyo nilishaingia kambini Itende, Mbeya.
Ni kwa juhudi zangu mwenyewe. Walau pale Itende JKT umeme uliwaka hangani mpaka saa nne usiku!
Usiku Mwema.
Maggid.

No comments:

Post a Comment