Wednesday, 15 April 2015

RIPOTI YA POLISI KUHUSU AJALI ZILIZOUA WATU 969 KWA SIKU 102



Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani DCP Mohammed Mpinga
Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani DCP Mohammed Mpinga
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akiungana na Watanzania kuomboleza vifo vya watu 19 walioteketea katika ajali ya basi lililoungua moto baada ya kugongana na lori juzi mjini Morogoro, imefahamika kuwa, ajali za barabarani zimegharimu maisha ya watu 969 kati ya Januari Mosi na Aprili 12 mwaka huu.
Aidha, watu 2,500 wamejeruhiwa katika kipindi hicho, wengine wakisababishiwa ulemavu wa kudumu kutokana na ajali hizo. Hii ina maana kwamba, kwa wastani, watu 10 walipoteza maisha katika ajali za barabarani kila siku kati ya Januari na Aprili 12 mwaka huu, ilhali waliojeruhiwa ni wastani wa watu 25 katika muda kama huo.
Hayo yalibainishwa jana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Mohammed Mpinga aliyesema hayo yametokea katika ajali za barabarani 2,224 za kati ya Januari na mwanzoni mwa Aprili.
Alisema watu 866 walikufa na wengine 2,363 kujeruhiwa kati ya Januari na Machi, wakati wengine 103 wamepoteza maisha na 138 kujeruhiwa kati ya Machi 11 na Aprili 12 mwaka huu.
Alisema katika ajali zote hizi chanzo kikubwa ni mwendokasi wa madereva bila kuzingatia alama na michoro ya barabarani na abiria kushabikia mwendo kasi na kumtetea dereva pindi anapofanya makosa.
"Dereva akifanya makosa akikamatwa abiria wanachangia kumlipia faini dereva jambo ambalo linawapa madereva kiburi wakiamini akifanya makosa abiria wanamsaidia," alisema Mpinga.
Aliongeza kuwa kwa upande mwingine wamiliki wa vyombo vya usafiri wanachangia ajali kwani wamekuwa wakiwadhibiti na kuwaamrisha madereva wao kwenda mwendo kasi na pale anapokosea anamlipia faini jambo ambalo linapelekea kutokea kwa ajali zinazopoteza maisha ya watu wengi na kuwaachia wengine vilema vya maisha.

No comments:

Post a Comment