Dar es
Salaam. Mama wa aliyekuwa nyota wa filamu nchini, marehemu Steven
Kanumba, Flora Mtegoa amesema kuwa kupitia Kampuni ya Kanumba The Great
Film inakamilisha uanzishaji wa taasisi itakayoitwa, Kanumba Foundation.
Pia,
alikanusha uvumi kuwa kampuni ya Kanumba imekufa, akifafanua jambo hilo
alisema kampuni hiyo inaendelea na shughuli zake. Alisema kutakuwapo
Kanumba Foundation ili kusaidia jamii wakiwamo wasanii katika masuala
mbalimbali.
Akizungumza
na gazeti hili, Flora alisema uamuzi wa kuanzisha taasisi hiyo ni
kuendeleza na kutimiza ndoto alizokuwanazo mtoto wake, marehemu Steven
Kanumba enzi za uhai wake.
"Tunaanzisha
Kanumba Foundation. Awali haikuwapo, tulivyojaribu kulikuwa na mlolongo
mrefu, marehemu Kanumba alikuwa na mipango mingi, huo ukiwemo. Kanumba
alisema akisharejea safari yake ya Marekani kuna vitu atafanya, lakini
Mungu akampenda zaidi," alisema Flora na kuongeza:
"Mipango
yake ilikuwa ni kuanzisha chuo kikubwa cha kufundisha sanaa ya uigizaji
kwa kuwachukua waigizaji chipukizi na kuwafunza ili wawe bora." Kuhusu
Kampuni ya Kanumba The Great, Mtegoa ambaye pia ni msanii alisema licha
ya kusema kuwa kampuni hiyo imekufa, lakini mpaka sasa imeweza
kutengeneza filamu kadhaa.
"Kampuni
ipo na bado naendelea kuisimamia. Kwa kipindi chote imetengeneza filamu
mbili ambazo zilishapelekwa sokoni tangu mwaka jana. Watu wengi
wanaamini kwamba ilifungwa, ila ipo na ina watu kama kawaida, japokuwa
ukipita nje unaona kama imefungwa," alisema. Flora maarufu kwa jina la
Mama Kanumba, alifafanua kwamba kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi za
watu wengine, pia inatengeneza filamu zake yenyewe. Alisema kutokana na
uwepo wa kampuni hiyo wameweza kufanya mambo mengi, ikiwamo kutimiza
ndoto za marehemu Kanumba za kuwa na mfuko wa jamii.
Akizungumzia
kipaji chake cha uigizaji, Mama Kanumba alisema hakufanya hivyo baada
ya mwanaye kufariki, bali alikuwa akiigiza wakati alipokuwa kigori,
hivyo ameamua kuendeleza kipaji chake.
"Nikiwa
sekondari niliigiza, wakati huo mtoto wa kike kupelekwa shule mpaka
vikao, zamani binti hakuruhusiwa kusoma, ilikuwa ngumu, kwa hiyo
unacheza huku ukifikiria kwamba nyumbani wakijua nimeingia huku itakuwa
tatizo, baadaye nikaacha," alisema.
Alisema baada ya Kanumba kufariki, aliamua kuendeleza kipaji chake kwa kutumia rasilimali alizoachiwa na mtoto wake.CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment