Friday, 25 July 2014

Tuliokuwepo mwaka 1979 bado tunakumbuka...!

nyerere_with_his_generals_on_amini_invasion_91658.jpg
Ndugu zangu,
Leo ni Siku ya Mashujaa. Nimeangalia TBC1 leo wakionyesha tukio lile la kihistoria pale nchi yetu ilipowapokea rasmi mashujaa wetu wa Vita Vya Kagera. Nilikuwa miongoni mwa watoto wale pale National Stadium. Nilikuwa na miaka 13 tu.
Ilikuwa ni siku ya ajabu, maana, shughuli nzima iliingia doa pale kwa macho yetu tuliposhuhudia ndege yetu ya kijeshi ikianguka na kuwaka moto. Hakika, rubani yule alifanya kazi ya kijasiri na kizalendo sana, maana, ingewezekana kabisa ndege ile kuangukia uwanjani na kusababisha madhara makubwa.
Nakumbuka kuiona ndege ile ikishuka huku ikitoa moshi, haikuwa jambo la kawaida. Hata katika umri wangu ule mdogo, nikahisi kuna kitu hakijaenda sawa. Mara tukaona ikikwepa kuangukia uwanjani na kuanguka nje ya uwanja.(P.T)
Nakumbubuka kushuhudia uwanja ukikumbwa na butwaa, mara zikasikika sauti za watu wakipiga kelele, kuna tulioanza kukimbilia eneo la tukio, kwa shauku ya kujua nini kimetokea, nami nilikuwa mmoja wao. Lakini sikufika mbali, nikarudi nilikosimama, chini na jirani na jukwaa kubwa.
Na hata aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Rashid Kawawa, alikuwa ni mmoja wa viongozi walioshuka jukwaani akikimbia, naye alionekana aliyeshtushwa, na pengine alilazimika kushuka jukwaani kwa vile alikuwa ni waziri mwenye dhamana ya Ulinzi. Rashid Kawawa alikuwa akiwajibika kwenye kazi yake.
Sura ya Rais, Julius Nyererere ilikuwa imevaa huzuni kubwa. Na aliposimama kuzungumza, napo ilikuwa ajabu kwangu katika umri ule, kuwa Julius Nyerere hakusema lolote juu ya tukio lile.
Lakini hii leo, nilipokuwa nikiangalia tukio la siku ile kupitia TBC1, nimekuwa mwelewa zaidi, kuwa Julius Nyerere alisiama kama Mkuu wa Nchi, alilijumuisha tukio lile na mashujaa wengine waliojitoa muhanga kwa ajili ya nchi yetu. Julius Nyerere hakushuka chini na kuzungumzia tukio la kuanguka kwa ndege ile. Badala yake,alitoa hotuba muhimu kwa taifa baada ya vita. Na ni katika siku ile Julius Nyerere alitangaza miezi kumi na nane ya kufunga mkanda.
Na hakika, makovu ya kiuchumi ya Vita Vya Kagera yangalipo mpaka hii leo. Naam, Vita Si Lelemama.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment