Tuesday, 15 July 2014

Neno Fupi La Leo; Kuna Ndoto Ya Urais Na Ndoto Ya Taifa...

Ndugu zangu,
Nimeandika juzi, kuwa nchi yetu haina uhaba wa wagombea urais, na kwenye moja ya magazeti ya leo, wametajwa wanaoweza kugombea kuwa ni kumi na mmoja, kama kikosi cha kucheza mechi kwenye Kombe la Dunia!
Si kugombea tu, kwamba kimsingi yeyote anaweza kugombea Urais. Kwenye siku ya Saba Saba mwaka huu nilikuwa kijijini Idodi, Pawaga. Pale niliwaona watoto hao pichani wakisubiri kwa hamu kuongalia kitakachoonyeshwa kwenye KwanzaJamii Cinema. Ilikuwa ni marudio tu ya mechi za Kombe la Dunia, lakini, wengi walikusanyika, kuangalia.
Kwa kuangalia watoto hao nilitafakari sana kuhusu nchi yetu, kwamba pamoja na hali duni za watu wetu wengi, yumkini tuna Watanzania miongoni mwetu wenye ndoto za kuwa marais kwa kudhani ni kazi rahisi sana, na kwa nchi yetu, hakuna pia uhaba wa ndoto za urais. Tatizo letu kama Taifa ni ukweli kuwa hatuna NDOTO ya TAIFA. Kwamba tunataka nini kama taifa.(P.T)
Na kama tungelikuwa na ndoto ya taifa, basi, na wenye ndoto za urais nao wangepungua, maana, mwenye kuota ndoto ya urais angelazimika pia kujiuliza swali muhimu; " Je, mimi natosha kwenye kuyatimiza yale yaliyomo kwenye ndoto ya taifa?"
Na kwa vile hatuna ndoto ya taifa, tusije tukashangaa siku moja, kuwa idadi ya watakaochukua fomu kugombea urais kufikia hata idadi ya kikosi kinachoruhusiwa na FIFA kwenda kushiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia; wachezaji 23, hivyo basi, wagombea urais 23!
Ni Neno Fupi La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.

Tuma Maoni

No comments:

Post a Comment