Saturday, 21 June 2014

Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi waipinga bajeti


.

Kangi Lugola 66669
Na Hudugu Ng'amilo
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi jana waliipinga hadharani bajeti ya Serikali inayoendelea kujadiliwa bungeni, kwa madai hawatakuwa tayari kuiunga mkono kwa kuwa haina jipya.
Wabunge hao ni Anne Kilango (Same Mashariki), Kangi Lugola (Mwibara) na Mbunge wa Viti Maalumu Vicky Kamata ambao kwa nyakati tofauti walisema kuunga mkono bajeti hiyo ambayo haitekelezeki ni sawa na kuwasaliti wananchi wao.
Lugola alitoa sababu za kutounga mkono bajeti hiyo kwa kuwa ni 'bajeti mchepuko' yenye vipaumbele lukuki lakini havitekelezi hata kimoja.
Mbunge huyo alitoa sababu zaidi ya saba za kutounga mkono, akisema ni mwiko kwa mbunge makini kuunga mkono bajeti kama ilivyo sasa kwa kuwa anatambua hakuna kitakachofanyika wakati wote wa utekelezaji.
"Nimeipa jina la bajeti mchepuko kwa sababu nyingi, la muhimu ni kuwa bajeti hii imejaza vipaumbele vingi ambavyo kwa mtazamo wangu havitatekelezeka hata siku moja," alisema Lugola.
Niweke wazi tu hapa kuwa, kama mtalazimisha mambo mengine ikiwamo misamaha ya kodi, nitakuwa tayari kutumia ubaunsa wangu humu ndani kupambana na mbunge yeyote anayepinga kufutwa kwa misamaha ya kodi,"alisema Lugola.
"Kama hamtaleta sheria ili tumpe meno kamishina wa madini, nakwenda Mwibara kuwahamasisha wavuvi siku mkiwakamata na nyavu au makokoro wagome hadi uchunguzi ufanyike kwanza."
Kwa upande wake, Vick Kamata alitoa sababu za kutounga mkono ni kutokana na kile alichokiita udanganyifu wa Serikali kwa wachimbaji wadogo ambao wameshindwa kupata msaada wakati wote.
Alisema Serikali imekuwa ikiwatengea maeneo ambayo hayana dhahabu kabisa na matokeo yake wanachimba hadi wanazeeka bila ya kupata dhahabu wakati ikiendelea kuwabeba wakubwa na matajiri.
Naye Kilango alisema sababu kuu ya kupinga ni hadi pale Serikali itakapoongeza fedha katika Wizara ya Afya ili iweze kulinda afya za Watanzania wanyonge wakiwamo akina mama na watoto jimboni kwake.
CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment