Friday, 27 June 2014

Balaa la kiuchumi lazidi kumwandama Luis Suarez



Luis-Suarez-Bite-in-2014-World-Cup-vs-Italy_57f58.jpg
Na Fadhy Mtanga 27 Juni 2014
Wakati anatakiwa kulipa faini ya paundi 64, 000/= kama sehemu ya adhabu ya FIFA, makampuni yameanza kuvunja mkataba na nyota huyo wa Uruguay.
Kampuni ya kamari ya 888 kutoka Gilbraltar imevunja rasmi mahusiano yake ya kibiashara na nyota huyo. Tayari kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas imeondoa matangazo yote ya Kombe la Dunia yenye picha za Luis Suarez. Adidas pia wamesema watapitia upya mahusiano yao ya kibiashara na nyota huyo mara baada ya kumalizika kwa fainali zinazoendelea nchini Brazil. Adidas ni washirika wakubwa sana wa FIFA. Katika taarifa yao, wamesema wanaiunga mkono FIFA.
Kampuni ya vifaa vya michezo ya Warrior Football inayotengeneza jezi zinazotumiwa na Liverpool nayo ipo katika mchakato wa ndani wa kufanya maamuzi juu ya uhusiano wake kibiashara na nyota huyo.
Wadhamini wa fulana za Liverpool, Standard Chartered wanatarajiwa pia kutoa msimamo wao.
Klabu ya Barcelona inatumia mwanya wa adhabu ya Suarez kumshusha dau hadi paundi milioni 50 kutoka bei yake kabla ya sakata ya paundi milioni 87.5
Luis Suarez amepigwa kufuri la kutojihusisha na kandanda kwa miezi minne, kutocheza mechi 9 za kimataifa baada ya kupatikana na hatia ya kumpiga meno mlinzi wa Italy mataifa hayo yalipokwaana katika michuano ya Kombe la Dunia mapema wiki hii.(P.T)

No comments:

Post a Comment