LOWASSA AANIKA UTAJIRI WAKE
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa,
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Spika Anne Makinda katika picha ya pamoja
iliyopigwa hivikaribuni
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema madai kwamba yeye ni
tajiri hayana ukweli wowote.
Amesema yeye ni mfugaji na anamiliki ng’ombe zaidi ya 800 katika Jimbo la Monduli, mkoani Arusha.
Lowassa alisema hayo katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake wiki iliyopita mjini Dodoma.
“Haya madai hayana hata chembe ya ukweli
hata kidogo, isipokuwa mimi nadhani wananitakia mema kwa sababu ukiona
jumba zuri wanasema la Lowassa, gari nzuri la Lowassa, kitu chochote
kizuri wanasema cha Lowassa,” alisema na kuongeza:
“Wamesema uongo mwingi sana, mimi nasema
tu nilichopata nimepata na sina utajiri kiasi hicho, lakini si
mbadhirifu wa haki zangu ninazopata kama mshahara na haki nyingine.”
Alipotakiwa kutaja mali anazomiliki, Lowassa alisema: “Mimi ni mfugaji, nina ng’ombe zaidi ya 800 jimboni kwangu Monduli.”
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli,
alisema madai kwamba anamiliki utajiri uliopindukia yalianza kabla
hajajiuzulu uwaziri mkuu na ilielezwa kuwa “maduka fulani” ni yake.
Alibainisha kuwa hata kampuni ya
Alphatel ambayo wanamiliki kwenye familia yake iliwahi kuhusishwa na
jengo kubwa lililojengwa na mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam likiitwa Alpha.
“Ikaonekana ni jengo langu, kule Mbezi kuna rafiki yangu mmoja walienda
watu wakasema hii nyumba ya Lowassa. Yule bwana alitoka na bastola
akawakimbiza. Mimi sina nyumba maeneo hayo,” alisema Lowassa.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment